Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ibrahim Zakzaky, siku ya Jumamosi, tarehe 17 Oktoba 2026 (25 Mehr 1405), alitoa ufafanuzi kuhusu wajibu wa vijana katika njia ya Harakati ya Kiislamu na maana ya kuisimamisha dini, wakati wa hafla ya kufunga Kongamano la Kimataifa lililokuwa na mada isemayo “Vijana na Mustakabali wa Harakati ya Kiislamu”, lililofanyika Abuja, mji mkuu wa Nigeria. Kongamano hilo liliandaliwa na taasisi ya Jeshi la Shahidi Ahmad Zakzaky (JASAZ).
Akizungumzia umuhimu wa kipindi cha ujana katika maisha ya mwanadamu, alisisitiza ulazima wa kutumia fursa hiyo katika kufanya shughuli zenye thamani na kutekeleza ibada. Alisema: “Kipindi cha ujana si miaka michache tu katika umri wa mwanadamu, bali ni kipindi cha uwezo na juhudi.”
Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria aliendelea kwa kukosoa baadhi ya mitazamo inayodai kuwa haiwezekani kuisimamisha dini kutokana na ukosefu wa rasilimali na nguvu, au kwa sababu si watu wote katika jamii ni Waislamu. Alisisitiza kuwa mtazamo wa aina hiyo hauwakilishi uelewa sahihi wa maana ya kuisimamisha dini.
Sheikh Zakzaky, akitofautisha kati ya kuisimamisha dini na kuwafanya watu wote katika jamii kuwa Waislamu, alisema: “Harakati yetu haiwaiti watu kwenye Ushia, bali inawaalika kuisimamisha dini.”
Akifafanua zaidi mtazamo huo, alisema kuwa; kuisimamisha dini kunamaanisha kuweka sheria za Mwenyezi Mungu kuwa ndizo zinazotawala na kuzuia kutungwa kwa sheria zinazokinzana na hukumu Zake. Alieleza kuwa mfumo wa Kiislamu unapaswa kujengwa kwa kuzingatia sheria za Mwenyezi Mungu na kutokinzana nazo.
Ili kufafanua suala hilo, Sheikh Zakzaky alirejelea uzoefu wa Sheikh Uthman bin Fodio na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Alikumbusha kuwa hata nchini Iran wapo wafuasi wa dini nyingine, wakiwemo Wayahudi. Kwa msingi huo, alisisitiza kuwa kuwafanya watu wote kuwa Waislamu si sharti la kuanzishwa mfumo wa Kiislamu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria, huku akizungumzia juhudi za maadui za kuikandamiza Harakati ya Kiislamu, alisema kuwa juhudi hizo hazitafanikiwa na kwamba ushindi utakuwa wa Harakati hiyo na njia ya haki.
Mwisho wa hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa kusimama imara katika kuunga mkono haki na ukweli. Aliwataka wananchi wasitosheke na kubaki watazamaji tu, bali wachukue misimamo na kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuisimamisha dini ya Mwenyezi Mungu.
Maoni yako